Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) limetangaza orodha mpya ya timu bora duniani kwa mwaka 2026, ambapo Tanzania imepanda nafasi, ikiendelea kuimarisha hadhi yake katika soka la kimataifa. Orodha hiyo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na matokeo ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Morocco wameongoza kwa kupanda kwa kiwango kikubwa zaidi barani Afrika, wakifikia nafasi ya nane duniani licha ya kupoteza fainali ya AFCON dhidi ya Senegal. Senegal nao wamepanda hadi nafasi ya 12 kutoka nafasi ya 17 waliyokuwa nayo mwaka 2024. Morocco mwaka jana walikuwa nafasi ya 11, huku nafasi yao bora kuwahi kushika ikiwa ya 10 mwaka 1998.
Kwa timu nyingine za Afrika, Nigeria waliomaliza nafasi ya tatu AFCON wameorodheshwa nafasi ya 26, Misri wako nafasi ya 31, Cameroon nafasi ya 45, huku Gabon wakishuka hadi nafasi ya 86 baada ya kutolewa mapema. Katika orodha ya jumla, Hispania wanaongoza duniani wakifuatiwa na Argentina, Ufaransa, England na Brazil, huku Ureno na Uholanzi wakishika nafasi ya sita na saba mtawalia.






