Bunge la Ulaya limepitisha pingamizi dhidi ya mpango wa Tume ya Ulaya wa kuelekeza msaada wa kifedha kwenda Tanzania kupitia mfuko wa NDICI-Global Europe hatua inayotajwa kuchochewa na hali ya kisiasa inayoendelea Nchini Tanzania.
Hatua hiyo imekuja baada ya matokeo ya kura zilizopigwa na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya juu ya kuzuia utekelezaji wa mpango huo ambapo kura 53 zilikubali pingamizi hilo huku 2 zikipinga wakati kura moja ikiharibika.
Awali tume ya Ulaya ilipanga kutuma zaidi ya Euro Milioni 150 kwenda Tanzania mwaka 2026, kwa ajili ya miradi ya maendeleo Nchini Tanzania ambapo utekelezaji wa msaada huo haukuzingatia hali halisi ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, David McAllister amesema uamuzi huo ni ishara ya wazi kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuendelea kutoa fedha kwa misingi ya nyaraka zinazopuuza hali ya ukandamizaji wa kisiasa, uchaguzi usio wa haki, na mwenendo wa kiimla wa Serikali.





