
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam.
Kesi hiyo imepangwa leo Septemba 8 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali mbele ya Jaji Dunstan Ndunguru huku upande wa Jamhuri ukitarajia kuwaita Mashahidi 30 kutoa ushahidi dhidi ya Lissu na kuwasilisha vielelezo 16.
Itakumbukwa awali kesi hiyo ilikuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baada ya kukamilishwa kwa upelelezi ikahamishiwa rasmi katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na hatua zaidi za kisheria.
Katika kesi hiyo ya uhaini Lissu anadaiwa Aprili 3, 2025 Jijini Dar es salaam alitengeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.